Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Kicheko wakulima wa kahawa TCB ikitangaza bei mpya elekezi

Muktasari:

  • Bei hiyo ya Sh11,500 kwa kilo ni kwa kahawa iliyochakatwa kwenye viwanda vidogo vilivyopo kwenye vyama vya ushirika (CPU), huku iliyochakatwa majumbani (HP) bei yake ikipanda kutoka  Sh8,500 hadi Sh9,000.

Moshi. Bodi ya Kahawa Tanzania (TCB) imetangaza bei elekezi ya zao la kahawa, kahawa ghafi ya Arabika (CPU-parchment) imepanda kutoka Sh10,000 iliyokuwepo msimu uliopita hadi kufikia Sh11,500 kwa kilo.

Bei hiyo ya Sh11,500 kwa kilo ni kwa kahawa iliyochakatwa kwenye viwanda vidogo vilivyopo kwenye vyama vya ushirika (CPU) huku iliyochakatwa nyumbani (HP) bei yake ikipanda kutoka Sh8,500 hadi Sh9,000.

Kahawa ghafi ya Robusta (Dry Cherry) bei yake ni Sh4,800 kwa kilo moja huku kahawa ghafi ya Arabika ngumu ikiwa ni Sh5,000.

Kwa mujibu wa Taarifa iliyotolewa na Mkurugenzi Mkuu wa TCB, Primus Kimaryo bei hizo zinajumuisha michango, Tozo (zinazolipwa na mnunuzi) na gharama nyingine za kibiashara.

"Bodi ya kahawa inawaelekeza viongozi wote na  vyama vya ushirika vya msingi vya kahawa (Amcos), halmashauri za wilaya na wanunuzi kuwa bei elekezi ya mauzo ya kahawa ghafi ya Arabika  (CPU-Parchment)  itakuwa ni Sh11,500 na kwa kahawa ghafi Arabika majumbani (HP) bei itakuwa Sh9,000 kwa kilo moja,” amesema Kimaryo.

Aidha, amesema bei hiyo itakuwa inafanyiwa marejeo mara kwa mara kuendana na mwenendo wa soko la dunia.

Akizungumza na Mkurugenzi wa Ubora na Masoko TCB, Frank Nyarus amesema bei nzuri ya kahawa inatokana na mwenendo wa bei katika soko la dunia na ubora wa kahawa husika.

"Kahawa inauzwa kutokana na ubora na ubora wa kahawa unazingatiwa wakati wa kutengeneza bei elekezi na kwa msimu huu, ambapo tumeshatangaza kuanza kwa msimu katika maeneo mbalimbali kutokana na kahawa inapokuwa imeiva na kwa sababu manunuzi yameshaanza tayari tumetangaza bei elekezi," amesema Nyarus.

Mkurugenzi wa ubora na Masoko TCB, Frank Nyarus

Ameongeza kuwa; "Tuwatake wakulima kuendelea kutayarisha kahawa yao kwa kuzingatia ubora kwa sababu wanapoandaa kahawa kwa ubora, bei inazidi kuongezeka. Kahawa inauzwa kutokana na ubora wa kahawa husika."

Aidha, amesema msimu wa ununuzi tayari umeanza na kuwataka wanunuzi kuomba leseni ambazo zitawawezesha kwenda kununua kahawa na kwamba mifumo itakayotumika ni ile iliyotumika msimu uliopita.

Akizungumzia msimu ambao unamalizika, Nyarus amesema mpaka sasa wameshauza kahawa safi tani 72,000 ambayo imeingiza zaidi ya Dola 300 milioni (Sh7.96 bilioni).

"Mfumo wa mauzo ya kahawa bado haujaisha, utaenda hadi Juni 30, 2025,” amesema.

Kuhusu uzalishaji wa kahawa, Nyarus amesema katika msimu wa 2025/2026 wanatarajia kahawa itakayozalishwa itakuwa Tani 80,000 na kuwataka wakulima kuendelea kuwekeza katika zao hilo na kuzingatia ubora.

"Tuwatake wakulima kuendelea kuwekeza kwenye zao la kahawa kwa kuwa kahawa inalipa, lakini pia niwatake wazingatie kanuni za ubora,” amesema.

Amesema wana mkakati wa kuongeza uzalishaji wa kahawa na moja ya mikakati hiyo ni jitihada mbalimbali zinazofanywa na bodi kwa kushirikiana na wadau ikiwemo kugawa bure miche bora ya kahawa kwa wakulima na kutoa elimu ya uzalishaji wa kahawa bora.

 "Lakini pia tunahamasisha wakulima kuiweka vyema miti ya kahawa ili istawi na kuzaa kwa wingi hasa ile miti ambayo imekuwa mizee ambayo haizai tena kwa ufanisi,” amesema.

Frank Mongi ambaye ni mkulima wa kahawa Wilaya ya Moshi, amesema kupanda kwa bei ya zao hilo ni matumaini mapya kwa mkulima na kwamba itamfanya kila mkulima kukimbilia kulima zao hilo.

"Zipo mbegu za kahawa zilizofanyiwa utafiti  ni nzuri na zinazaa kwa wingi, na mkulima akizingatia ubora anapata bei nzuri sokoni, hivyo kuambiwa bei imefika Sh11,500 ni faraja kwa wakulima," amesema.

mmoja wa wakulima wa zao hilo wilayani Rombo,  Catherine Ndagu  amesema bei mpya ya kahawa itawatia motisha wakulima kwa kuwa baadhi yao walikuwa wameshakata tamaa kulima zao hilo.

"Bei hii mpya ya kahawa kwa kweli imetupa moyo wa kuendelea kulima kahawa, imetupa nguvu ya kuongeza juhudi kwenye uzalishaji, maana kuna kipindi tulikata tamaa kwa kweli lakini tunaamini kwa bei hii mpya watu watakimbilia kwenye kilimo hiki," amesema mkulima huyo.


OSZAR »