JKT yawaita waliomaliza kidato cha sita, vigezo hivi hapa

Kaimu Mkuu wa Tawi la utawala JKT, Kanali Juma Mrai akizungumza na waandishi wa habari Jijini Dodoma. Picha na Hamis Mniha
Muktasari:
- Wakati vijana wa kidato cha sita wamehitimu masomo yao, Jeshi la kujenga Taifa (JKT) limewaita kwenda katika mafunzo kwa mujibu wa sheria.
Dodoma. Jeshi la Kujenga Taifa (JKT), limewaita vijana waliomaliza kidato cha sita mwaka 2025 kuhudhuria mafunzo ya JKT kwa Mujibu wa Sheria kwa mwaka 2025.
Kwa mujibu wa JKT, vijana hao wanatakiwa kufika katika makambi waliyopangiwa kati ya Mei 28 hadi Juni 8,2025.
Hayo yamesemwa leo Jumanne, Mei 27,2025 na Kaimu Mkuu wa Tawi la Utawala JKT, Kanali Juma Mrai alipokuwa akizungumzia wito huo kwa niaba ya Mkuu wa JKT Meja Jenerali Rajabu Mabele.
Vijana hao wamepangiwa kuripoti katika makambi ya JKT Rwamkoma (Mara), Msange (Tabora), Ruvu na Kibiti (Pwani), Mpwapwa na Makutopora (Dodoma).
Kambi nyingine za JKT ni Mafinga (Iringa), Mlale (Ruvuma)Mpambo na Maramba (Tanga), Makuyuni na Orjolo (Arusha), Bulombora, Kanembwa na Mtabila (Kigoma), Itaka (Songwe) Luwa na Milundikwa (Rukwa), pamoja na Nachingwea (Lindi).
“Wahitimu wenye ulemavu wa kuonekana kwa macho (physical disabilities) waripoti katika kambi ya Ruvu iliyo Mlandizi mkoani Pwani ambayo ina miundombinu ya kuhudumia watu wa jamii hiyo,”amesema.
Kanali Mrai amewataka vijana hao kuripoti wakiwa na bukta rangi ya bluu iliyokoza yenye mpira kiunoni iliyo na mfuko mmoja wa nyuma, urefu unaoishia magotini isiyo na zipu.
Vifaa vingine wanavyotakiwa kwenda navyo ni fulana ya rangi ya kijani, raba za michezo zenye rangi ya kijani na bluu, shuka mbili za kulalia zenye rangi ya bluu bahari na soksi ndefu za rangi nyeusi.
Vitu vingine ambavyo vinatakiwa ni nguo za kuzuia baridi kwa waliopangiwa mikoa yenye baridi, traki suti ya rangi ya kijani au bluu.
Kanali Mrai ametaja vingine kuwa ni nyaraka zote zinazohitajika katika udahili wa kujiunga na elimu ya juu zikiwemo cheti cha kuzaliwa, vyeti vya kuhitimu kidato cha nne na nauli ya kwenda kuripoti kambini na kurudi nyumbani.
Amesema kuwa orodha kamili ya majina ya vijana hao, makambi ya JKT waliyopangiwa na maeneo ambayo makambi hayo yalipo na vifaa na vifaa wanavyotakiwa kwenda navyo, inapatikana katika tovuti ya JKT ambayo ni www.jkt.militz
Amesema ili kufahamu kambi kijana aliyopangiwa, atatakiwa kuingiza jina la shule na namba ya shule aliyohitimu elimu ya kidato cha sita mbele ya jina lake la shule yake ataona neno lililoandikwa waliochaguliwa.
Kanali Mrai amesema kijana akichagua neno hilo ataona jina na majina ya waliochaguliwa na mafunzo kwa Mujibu wa Sheria kwa mwaka 2025 ikionyesha kambi aliyopangiwa, mkoa na wilaya iliyoko katika kambi husika.
“Mkuu wa JKT Meja Jenarali Rajabu Mabele anawakaribisha vijana wote waliohitimu kidato cha sita mwaka 2025 kuungana na vijana wenzao ili kujengewa uzalendo, umoja wa kitaifa kufundishwa stadi za kazi, stadi za maisha na utayari wa kulijenga na kulitumikia Taifa lao,”amesema.
Akiwasilisha bajeti ya mwaka 2025/26, Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Dk Stergomena Tax alisema katika kuhakikisha kuwa, wahitimu wote wa kidato cha sita wanapata fursa ya kujiunga na mafunzo ya JKT, miundombinu ya makambi imeendelea kuboreshwa.
Alisema hadi mwaka 2025 JKT imefikia uwezo wa kuchukua vijana 60,000 ikilinganishwa na uwezo wa kuchukua vijana 40,000 mwaka 2021.