Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Utata kifo cha raia anayedaiwa kugongwa na gari la Maliasili

Muktasari:

  • Askari wa Maliasili wanadaiwa kumuua mwanakijiji kisha mwili kuzikwa haraka kwa gharama za Serikali. RPC adai amekufa kwa ajali, ndugu wacharukaMkuu wa Wilaya aagiza wahusika wawekwe ndani.

Dar es Salaam. Maofisa wa Maliasili wilayani Kibiti mkoani Pwani, wanadaiwa kumuua Haji Mnette na kuuzika mwili wake haraka kupoteza ushahidi, nduguze wamelalamika.

Mkuu wa Wilaya ya Kibiti, Kanali Joseph Kolombo ameagiza wahusika wawekwe ndani na wananchi wawe watulivu wakati suala hilo likifanyiwa kazi.

Mnette anadaiwa kuuawa baada ya kugongwa na gari la watumishi hao, waliokuwa wakimfukuzia katika msitu wa Ngulakula.

Hata hivyo, Kamanda Msaidizi wa Polisi Kanda Maalumu ya Rufiji, Kanuti Msaki amesema: “Mbona hajagongwa na gari? Huyo mwananchi alikuwa anaendesha pikipiki, akakutana na gari la Maliasili wakawa wanapishana.

“Wakati gari la Maliasili likiwa limeenda mbele kugeuka lirudi na barabara, yule mwananchi akafikiria linamfukuza, akaanza kukimbia ndipo alikutana na tuta, pikipiki ikamshinda akaanguka na kupasuka kichwa,” amesema Kamanda Msaki.

Kamanda Msaki, alisema taarifa hiyo ilipelekwa kwake na askari wake baada ya kwenda eneo la tukio, ingawa bado jeshi hilo linaendelea kuwahoji watu wa Maliasili wanaotuhumiwa ili kupata majibu sahihi.

Tukio hilo lilitokea Jumanne Mei 27, 2028 saa moja asubuhim wakati Mnette aliyekuwa akiendesha pikipiki kudaiwa kugongwa na gari hilo, lililosababisha kifo chake.

Kaka mkubwa wa Mnette, Rashid Mkamba ameliambia Mwananchi kuwa tukio hilo lilitokea wakati ndugu yake anatoka porini eneo la Ngulakula kuchukua vipande vya mbao, vinavyotumika kutengenezea mbuzi za kukunia nazi, ambavyo havikulipiwa kibali.

Mkamba amesema Mnette akiwa njiani kuelekea Kibiti Mjini, akikaribia eneo lenye barabara ya vumbi ya kutoka Ngulakula, alipokutana na maofisa hao walioanza kumkimbiza kwa nyuma kwa kutumia gari ili kumtia nguvuni.

“Walifukuzana hadi kufikia sehemu ambayo kulikuwa na kona pamoja na tuta, ambapo Mnete alijaribu kufunga breki ili kupunguza mwendo kwa ajili ya kukata kona eneo la Mwangia, ndipo gari la maofisa hao lilipomgonga kwa nyuma.

“Wamekamatwa wanahojiwa hadi sasa kujua ukweli uko namna gani na ikithibitika tutawaambia,” amesema.

Hata hivyo, Mnette amesisitiza: “Baada ya kumgonga Mnette alirushwa kutoka kwenye pikipiki na kuvunjika mshipa wa shingo na kusababisha kifo chake papo hapo.”

Kwa mujibu wa Mkamba, baada ya tukio hilo inadaiwa askari walichukua mwili wa Mnete kuupeleka hospitali kwa ajili ya vipimo.

“Tulipewa kibali na Serikali imekubali kugharimia mazishi (yaliyofanyika jana). Maiti imetolewa kwenda kuzikwa Kijiji cha Mtunga nyumbani kwa marehemu, magari kila kitu wanatumia vya kwao (Serikali),” amesema.

Hata hivyo, Mkamba anasema baada ya tukio hilo kulitokea tafrani kubwa kwa wananchi wa Kibiti, ndipo walipochukua uamuzi wa kwenda kwa mkuu wa wilaya ya Kibiti.

“Tulikwenda kwa mkuu wa wilaya kulalamika, tukihitaji kujua kama Serikali itahudumia gharama za msiba, lakini marehemu alikuwa na madeni na familia ya mke na watoto wanne ambayo imekuwa ikimtegemea,” anasema.

Ndugu mwingine wa Mnette, Hamisi Mnette amesema wanasubiri taratibu za kiuchungu zifanyike ili waliohusika na tukio hilo kufikishwa katika vyombo vya dola.

“Kama watashindwa basi tutafuata sheria inavyosema, ili haki itendeke kwa ndugu yetu, maana ana familia na inaonekana wamemfanyika makusudi. Si sheria kumgonga mtu ili akamatwe kwa lazima wakati hajaua,” amesema Mnette.

Baada ya kutoa malalamiko hayo mkuu wa wilaya hiyo aliagiza mwili huo ukazikwe na kutoa amri kwa wale waliosababisha kifo wakamatwe pamoja na gari lipelekwe polisi.


DC aagiza uchunguzi

Mkuu huyo wa wilaya Kanali Joseph Kolombo amesema kwa sasa suala hilo linafanyiwa uchunguzi na Jeshi la Polisi ambalo lina mamlaka hayo.

“Tukio hilo lilitokea asubuhi, hakuna aliyeliona zaidi ya marehemu na wale waliokuwa doria, kwa hiyo linahitaji uchunguzi wa Polisi kujua kama aligongwa au hakugongwa, kwa sababu Mnette alikuwa kwenye pikipiki,” amesema.

“Tusubiri uchunguzi wa Polisi, jana nilikuwa na wananchi nimezungumza nao na kuwaambia wawe watulivu, tusubiria Polisi wanasemaje. Ni tukio baya la mtu kupoteza maisha,” amesema Kanali Kolombo.


OSZAR »