Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Bazecha watoa msimamo mtikisiko wa kisiasa Chadema

Muktasari:

  • Baraza hilo limetafsiri hatua ya baadhi ya makada wa chama kujivua nyadhifa zao na kuondoka kama hatua mojawapo inayopitiwa na bahari kutema uchafu.

Dar/Mikoani. Wakati makada wakiendelea kukihama Chadema kwa makundi, Baraza la Wazee la chama hicho (Bazecha), limeifananisha hatua hiyo sawa na bahari kuutema uchafu unapoingia baharini.

Mbali na hilo, Bazecha limesema chama hicho kipo imara kuliko wakati mwingine wowote. Pia tamaa ya nafasi za ubunge na udiwani inatajwa kuwa sababu ya hamahama inayoendelea.

Bazecha ikitoa kauli hiyo, wanaojiondoa wanasema hata chumvi ni sehemu ya uchafu unaotemwa na bahari, lakini ni kiungo muhimu kwenye mboga.

Wanasema kuondoka kwao kunafanya mboga ikose mlaji kwa kuwa haina tena ladha.

Bazecha ikitoa kauli hiyo, leo Mei 16, Mwenyekiti wa chama hicho Mkoa wa Dodoma, Aisha Madoga naye amebwaga manyanga akifuata nyayo za wengine waliojiondoa wakitaja sababu kadhaa zikiwamo za kukosa uhuru wa kutoa maoni na kuitwa wasaliti.

Miongoni wa waliojiondoa Chadema leo Mei 16 wamo makada wanaotajwa idadi yao kuwa 56 wa kutoka Mkoa wa Kigoma, wakidai mwenendo usioridhisha na kutosikilizwa kwa maoni ya wanachama ndio sababu.


Bahari inajisafisha

Katika mkutano na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam leo Mei 16, Mwenyekiti wa Bazecha Kanda ya Pwani, James Haule ameifananisha hamahama inayoshuhudiwa na tabia ya bahari kujisafisha pale inapoingiwa na uchafu.

"Baada ya kufuatilia tumegundua chama kipo imara kuliko wakati mwingine wowote, bahari inatema uchafu, hivyo nitoe wito anayeshuka kwenye basi amefika mwisho wa safari na siasa inasafari ndefu, hao wanaoshuka huenda wasifike nchi ya ahadi wanavyotaka kwenda na kuishia njiani," amesema.

Amesema ndani ya chama hicho hakuna majeraha kwa kuwa hayupo aliyelalamika.

"Huwezi kusema kuna majeraha kwa sababu hakuna aliyesema ana majeraha, tiba ya kukanyangana kila mtu anatibu majeraha yake," amesema.

Haule amesema ni jambo la kawaida kutokea mkanyangano wakati wa uchaguzi, hivyo kama yupo aliyekanyagwa anapaswa kutibu majeraha yake.

Amesema baada ya uchaguzi mkuu wa chama hicho (Januari 21, 2025), walikaa na viongozi wote na kuzungumza nao, hivyo hakuna majeraha bali suala la wanachama kuondoka ni demokrasia iliyopo ndani ya Chadema.


Majibu ya Mrema

Alipotafutwa na Mwananchi kuzungumzia kauli ya Bazecha, mmoja wa waliotangaza kukihama chama hicho, John Mrema amesema huo ni mwendelezo wa matusi yaliyokifikisha chama hicho kilipo sasa.

"Huyu ni mwenyekiti wa wazee ambaye alipaswa kuwa msuluhishi na muunganishi wa chama, Baraza la Wazee kaulimbiu yao ni “Kisima cha hekima na busara.

"Iko wapi hekima na busara, ndiyo maana tunasema chama chao kimepoteza mwelekeo, malengo na hakina tena sifa za kuwa chama cha kutetea haki na masilahi ya wananchi kama kinashindwa kulinda haki na masilahi ya wanachama wake," amesema.

Mrema aliyekuwa mkurugenzi wa itifaki na mambo ya nje wa chama hicho, amesema chumvi ni sehemu ya uchafu katika bahari, lakini ni kiungo muhimu.

"Hata chumvi ni sehemu ya uchafu unaotemwa na bahari ila ni kiungo muhimu sana kwenye mboga. Hajakosea kwani mboga huko hailiki maana haina ladha," amesema.


Ni tamaa tu

Licha ya sababu zinazotajwa na wanaohama Chadema, Makamu Mwenyekiti wa chama hicho Kanda ya Nyasa, Frank Mwakajoka amesema makada hao wamegubikwa na tamaa za uongozi na kwamba hata wakiondoka, hawawezi kuikwepa ajenda ya No reforms, No election.

“Hata kama wanataka nafasi za uongozi, hawawezi kukwepa hii ‘slogan’ ya No reforms, No election kwa kuwa wengi wao walikuwa kwenye sekretarieti na maofisa wa chama kwa miaka mingi.

“Wanaosema chama hiki kinaendeshwa na watu wawili, si kweli hili lililetwa kwenye Baraza Kuu na wao walikuwamo. Mkutano Mkuu wa chama ulipitisha sasa sijui mkutano mkuu unakuwa na watu wawili, huu ni uongo na ni vigumu kuwajibu,” amesema.

Amewajibu wanaodai chama hicho kitakufa kwa kutoshiriki uchaguzi mkuu Oktoba mwaka huu; akisema Chadema haiwezi kutetereka akitoa mfano yaliyotokea katika uchaguzi wa 2019 na 2020, ya wagombea wao kuenguliwa, kuwa bado walibaki imara.


Wajivua uanachama

Mwenyekiti wa chama hicho mkoani Dodoma, Aisha Madoga akitangaza kujiondoa katika chama amesema amefikia uamuzi huo kutokana na kukosekana uhuru wa kutoa maoni ndani ya Chadema na kuwa anayeyatoa anaitwa msaliti.

"Siondoki Chadema sababu nabishana na mtu, ila naondoka kwa sababu sitaki kubishana na chama, nakipenda sana changu," amesema.

Aliyekuwa Katibu wa Chadema Wilaya ya Kigoma Mjini, Deogratius Liyunga amesema pamoja na wenzake wameamua kuhama kutokana na mwenendo usioridhisha ndani ya chama hicho.

"Baada ya uchaguzi Mlimani City sisi timu mwamba (Freeman Mbowe), tumekuwa tukiandamwa kila ukitoa maoni au ushauri hausikilizwi sasa imebaki tunapokea maelekezo kutoka juu, hatuna haki katika chama ambacho nimekitumikia kwa muda mrefu," amesema.

Wengine waliotangaza kujiengua katika chama hicho ni Mwenyekiti wa Baraza la Wanawake Chadema (Bawacha) Mkoa wa Kigoma, Hadija Ramadhan na Dismas Wiston aliyekuwa mwenyekiti wa Jimbo la Kigoma Kaskazini.

Wamo pia viongozi wengine wa Bavicha na wa kata zilizopo katika majimbo ya Kigoma Mjini, Kigoma Kaskazini na Kigoma Kusini.


Heche achanja mbuga

Licha ya hayo, Makamu Mwenyekiti wa Chadema (Bara), John Heche ameendelea na ziara ya kunadi No reforms, No election. Akihutubia mikutano kwa nyakati tofauti Solwa na Mwakitolyo wilayani Shinyanga leo Mei 16, 2025, amesema Serikali inayoundwa na CCM inaogapa mabadiliko ya sheria kwa sababu yataondoa mianya inayotumika kukipendelea chama hicho tawala.

"Kila wakati viongozi wa CCM na Serikali wanadai Rais Samia Suluhu Hassan anaupiga mwingi, sasa wanaogopa nini? Warekebishe sheria na mfumo kuwezesha uchaguzi huru na haki kwa wagombea na vyama vyote," amesema

Amesisitiza msimamo wa chama chake wa kutoshiriki uchaguzi wowote katika mfumo na sheria zilizopo kwa sababu uzoefu wa chaguzi za mwaka 2019, 2020 na 2024 unadhihirisha kuwa wagombea kupitia vyama vya upinzani hawatatendewa haki.

Amefanananisha hali hiyo na mchezo wa soka, hususan timu za Simba na Yanga, kuwa hakuna inayoweza kukubali refa atoke kwa mpinzani wake, na kuwa ndiyo maana hata wao wanapinga wasimamizi wa uchaguzi kutoka chama tawala.

Mwenyekiti wa Baraza la Wazee la Chadema (Bazecha), Suzan Lyimo amewaomba wazee wote nchini kuunga mkono kampeni ya mabadiliko yatakayohakikisha viongozi wa kisiasa wanapatikana kwa haki kupitia kura za wananchi, hivyo kuwajibika kwa umma.

Amesema Serikali inayopatikana kwa nguvu ya kura itawajibika kwa wananchi kwa sababu viongozi watahofia kuwajibishwa wasipotimiza wajibu.

Mwenyekiti wa Baraza la Vijana la Chadema (Bavicha), Deogratius Mahinyila amewataka vijana nchini kuwa chachu ya mabadiliko akisema kote duniani, mabadiliko ya kweli huletwa na vijana na maskini wanaopigania maisha bora.

Katibu Mkuu wa Chadema, John Mnyika akihutubia wananchi wilayani Maswa, amesema baadhi ya wabunge wa Mkoa wa Simuyu wanamiliki kampuni za ununuzi wa pamba, huku wakitumia ushawishi wao bungeni na serikalini kushinikiza upangaji wa maeneo ya ununuzi uwape fursa ya kibiashara badala ya mkulima.

“Mkulima hawezi kupata bei nzuri ya pamba kutokana na wabunge wanaotoka katika maeneo yanayolima zao hilo kujihusisha na biashara ya zao hilo, hivyo wanatumia nafasi zao za kisiasa kuhakikisha wanapata faida huku mkulima akiwa anapewa bei ndogo,” amesema.

“Kwa sasa bei elekezi ya pamba iliyotangazwa na Serikali ni Sh1,150 ambayo ni ndogo ukilinganisha na gharama anazotumia mkulima hii ni kutokana na mfumo mbovu wa Serikali ambao sisi Chadema tunapigania kuuondoa,” amesema.


OSZAR »