Prime
Kamati Kuu Chaumma kujadili mambo haya…

Muktasari:
- Swali kuhusu kina nani watakaopewa ridhaa ya kupeperusha bendera ya Chaumma katika wadhifa wa urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Zanzibar, huenda likapatiwa jawabu kupitia kikao hicho cha Kamati Kuu.
Dar es Salaam. Chama cha Ukombozi wa Umma (Chaumma) kesho, Machi 24, 2025 kitafanya kikao chake cha kwanza cha Kamati Kuu tangu kupokea maelfu ya wanachama wapya waliotoka Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kikao kinachotarajiwa kuibua mageuzi makubwa katika muundo na falsafa ya chama hicho.
Mbali na mitazamo hiyo, taarifa rasmi ya chama hicho imeeleza kikao hicho kitakachofanyika jijini Dar es Salaam, kitakuwa na ajenda mbili ambazo ni kuchagua wakurugenzi wa idara makao makuu ya chama na kujadili na kupitisha ratiba ya ziara ya kitaifa.
Ziara hiyo, kwa mujibu wa taarifa hiyo, inalenga kutambulisha viongozi wapya wa ngazi ya Taifa, kupokea wanachama wapya, kueneza sera na kukiandaa chama hicho, kushiriki Uchaguzi Mkuu
Chama hicho, kilichojipambanua kwa sera ya ubwabwa shuleni na hospitali, kimekuwa gumzo kwa siku za karibuni kutokana na kunasibishwa na ukwasi usiomithirika, baada ya kufanya mikutano kadhaa inayotajwa kugharimu mamilioni ya fedha.
Maelfu ya wanachama hao ni wale walioihama Chadema kwa siku za karibuni, kwa kile walichoeleza kwa nyakati tofauti kuwa hawakuwa wanaridhishwa na mwenendo wa uongozi mpya wa chama hicho, hivyo kujiunga Chaumma kuendeleza siasa.
Swali kuhusu kina nani watakaopewa ridhaa ya kupeperusha bendera ya Chaumma katika wadhifa wa urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Zanzibar, huenda likapatiwa jawabu kupitia kikao hicho cha Kamati Kuu.
Kikao hicho pia kinatarajiwa kuja na muundo wa uongozi wa chama hicho kuanzia ngazi ya matawi hadi mikoa, kadhalika ngome zote za vijana, wazee na wanawake.
Ukiacha sera ya ubwabwa inayokitambulisha chama hicho, pengine Kamati Kuu ikaja na falsafa mpya itakachokipambanua Chaumma mbele ya jamii, hasa baada ya mabadiliko madogo ya uongozi wake wa kitaifa na kupokea wanachama wapya.
Ni mwendelezo wa kufuru kama ilivyokuwa katika vikao kadhaa ilivyovifanya siku za karibuni? Ndilo swali linalosubiri majibu kwa kitakachoshuhudiwa katika kikao hicho cha ngazi ya juu cha Chaumma.
Wagombea urais
Kikao hicho kinafanyika wakati ambao bado chama hicho hakijaamua wanachama gani watapeperusha bendera yake katika nafasi za urais wa Bara na Zanzibar katika Uchaguzi Mkuu wa Oktoba mwaka huu.
Ukiacha jina la Hashim Rungwe katika mbio za urais wa Bara, nyuma yake linatajwa jina la Mwenyekiti mstaafu wa Chadema, Freeman Mbowe, kuwa huenda akatokea kuwania urais kwa chama hicho.
Ingawa Mbowe hakuwahi kueleza popote wala kuwahi kushuhudiwa akijiunga na Chaumma, uhusiano wake na chama hicho unahusishwa na watu wake wa karibu kisiasa ambao wengi wamehamia huko.
Kama hiyo haitoshi, Mbowe anahusishwa na Chaumma kwa sababu hata mlinzi wake binafsi, Hassan Bwire, ameshuhudiwa katika mikutano yote ya chama hicho akiwalinda viongozi.
Sambamba na hayo, vishindo vya kisiasa walivyoanza navyo Chaumma vinakaribia kufanana na vile vya Mbowe, ikiwemo kutumia chopa kwa ajili ya ziara za viongozi mikoani.
Kubwa zaidi, anahusishwa hasa kutokana na chama hicho kilichokuwa dhoofu kiuchumi, lakini sasa kimeibuka ghafla na kumudu kila lililokishindwa zamani, hivyo wapo wanaodhani nyuma yake kuna Mbowe.
Ukiacha mitazamo ya jamii kuhusu Mbowe na Chaumma, mwanazuoni wa Chuo Kikuu cha Tumaini Dar es Salaam, Dk Lazaro Swai, amesema haitakuwa ajabu kumwona Mbowe ndani ya chama hicho.
Kauli yake hiyo inatokana na kile alichofafanua kuwa ni kawaida ya mwanasiasa yeyote na popote duniani kutafuta jukwaa la kutekeleza utashi wake.
Kwa sababu Chadema kwa sasa ina mambo yake, ameeleza inawezekana Mbowe akaonekana katika jukwaa lingine kutafuta fursa ya kutimiza ama malengo yake au utashi wake wa kisiasa.
“Mwanasiasa kila siku anatafuta jukwaa. Kwa maana hiyo, jukwaa lake la kisiasa lilikuwa Chadema na sasa ina mtu pale juu, kwa hiyo anachotazama ni kupata jukwaa lingine la siasa. Ili aendelee kufanya siasa, anapaswa kuwa na jukwaa la kutekeleza hilo na haitakuwa ajabu wala hatutashangaa tukiona akifanya hivyo,” amesema.
Wasiwasi wa Dk Swai ni kuaminika kwa jukwaa la Chaumma kama mbadala wa majukwaa mengine ya kisiasa.
“Unapochagua jukwaa, lazima uchague linaloaminika. Sijawa na uhakika kama Chaumma imekuwa credible kiasi gani,” amesema.
Katika maelezo yake hayo, amesema ukimya wa Mbowe unatia wasiwasi kuhusu uanachama wake ndani ya Chadema na pengine amesusa.
“Ukimya wake baada ya uchaguzi unakuwa kama amesusa, na kususa ni kukata tamaa, na nisingetarajia Mbowe awe hivyo,” amesema.
Kwa upande wa Zanzibar, Katibu Mkuu wa chama hicho, Salum Mwalimu, ndiye anayetajwa kuwa karibu na uteuzi wa kuwania urais kwa upande wa Zanzibar kwa sababu ana wasifu wa kuwahi kuwa mgombea mwenza wa urais katika uchaguzi wa 2020.
Alipotafutwa kuzungumzia hilo, Mbowe simu yake iliita bila kupokelewa, na hata alipotumiwa ujumbe hakujibu.
Muundo wa uongozi
Mwananchi Digital liliripoti kuhusu mpango wa chama hicho kukamilisha safu ya uongozi wake, kwa maana ya wajumbe wa sekretarieti wanaohusisha wakurugenzi wa idara mbalimbali za chama hicho.
Ukiacha nafasi hizo, Chaumma kabla ya kundi la wanachama wapya, ilikabiliwa na ombwe la uongozi katika baadhi ya ngazi, ikiwemo matawi, kata, wilaya na mikoa.
Kadhalika, hata uongozi wa ngome za chama hicho haukuwa unajulikana, hivyo kikao hicho kinatarajiwa kutoka na jawabu la swali hilo.
Naibu Katibu Mkuu wa chama hicho Bara, Benson Kigaila, ameiambia Mwananchi jana kuwa pamoja na mpango wa kusaka viongozi, pia chama hicho kinatafuta ofisi mpya.
Ofisi hiyo, kwa mujibu wa Kigaila, iwe angalau na uwezo wa kukidhi kurugenzi saba za chama hicho na maeneo mengine muhimu, yakiwemo ya mikutano, kuendana na hadhi ya chama hicho kwa sasa.
Katika kikao hicho, pengine hilo ni jambo lingine linalotarajiwa kujadiliwa.
Mabadiliko ya falsafa
Kwa miaka 13 tangu kuanzishwa kwake, Chaumma si miongoni mwa vyama vya upinzani vilivyoshuhudiwa vikifanya siasa za nginjanginja.
Pengine nguvu yake ya kiuchumi ilisadifu hilo, lakini hata kwenye majukwaa machache kiliyoyapata, wanasiasa wake walizungumza kwa lugha laini.
Kilipata umaarufu kiasi wakati wa Uchaguzi Mkuu 2020, mgombea wake wa urais na ndiye wa muda wote tangu kilipoanzishwa, Hashim Rungwe, alipokuja na sera ya ubwabwa shuleni na hospitali.
Umaarufu wake haukutokana na mapenzi ya jamii kwa sera husika, isipokuwa wengi waliitafsiri kama ucheshi.
Katika wakati huu ambao Chaumma imepata kundi kubwa la wanachama na angalau inajiweza kiuchumi, sera ya ubwabwa inaweza kuwepo, lakini isiwe ndiyo utambulisho wa chama hicho.
Kikao hicho kinatarajiwa, pamoja na ubwabwa, pia kije na sera mbadala itakayoitambulisha Chaumma na hatimaye jamii ikaelewa falsafa ya chama husika.
Akizungumzia hilo, mchambuzi wa masuala ya siasa, Kiama Mwaimu, amesema kwa hatua iliyopo sasa sera ya ubwabwa si stahiki kwa chama hicho.
Ameeleza itarajiwe ujio wa sera mbadala wa ubwabwa, ili kujenga ushawishi na mvuto kwa wanasiasa wengine.
“Ile falsafa yao ya ubwabwa haifai, itarajiwe mpya,” amesema Mwaimu.