Madeleka ajitosa ubunge Kivule, aapa kumaliza changamoto

Muktasari:
- Madeleka ametia nia katika jimbo hilo jipya limepatikana baada ya kugawanywa kwa Jimbo la Ukonga ikiwa ni miongoni mwa majimbo manane mapya yaliyotangazwa na Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC), Mei 12, 2025.
Dar es Salaam. Kada wa ACT Wazalendo, Peter Madeleka amechukua fomu ya kuomba ridhaa ya kuwania ubunge katika Jimbo la Kivule kwa tiketi ya chama hicho katika uchaguzi mkuu wa Oktoba 2025.
Madeleka ametia nia katika jimbo hilo jipya limepatikana baada ya kugawanywa kwa Jimbo la Ukonga ikiwa ni miongoni mwa majimbo manane mapya yaliyotangazwa na Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC), Mei 12, 2025.
Madeleka ametimiza siku 11 leo tangu amejiunga rasmi na chama hicho, Mei 20, 2025 na kukabidhiwa kadi ya uanachama na Makamu Mwenyekiti wa ACT Wazalendo, Isihaka Mshinjita, baada ya kukihama Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema).

Madeleka ambaye pia ni wakili wa kujitegemea, aliondoka Chadema akipingana na msimamo wake wa chama wa “No reforms, no election” (bila mabadiliko, hakuna Uchaguzi) unaolenga kuishinikiza mabadiliko katika mifumo ya uchaguzi.
Akizungumza baada ya kuchukua fomu katika ofisi za chama hicho, Kivule na kukabidhiwa fomu na katibu wa kimbo hilo, Emmanuel Magoto, Madeleka amesema iwapo atateuliwa na chama hicho na akafanikiwa kushinda, basi kipaumbele chake ni kushughulika na shida za wananchi.
“Kivule ni kati ya maeneo yaliyosahaulika kihuduma kama maji, umeme, barabara. Nikiteuliwa na chama changu na wananchi wakinichagua kwa kunipigia kura, nikafanikiwa kuingia bungeni, nitaanza kushughulika na changamoto hizo,” amesema.
Amesema Kivule ni nyumbani kwake kwa kuwa wamekuwa wakilalamika kwa muda mrefu na hiyo ndiyo sababu iliyomsukuma zaidi kuomba ridhaa hiyo kupitia chama chake.
“Nchi yetu ina matatizo mengi na kunahitajika mabadiliko lakini mabadiliko hayo tutayapata ndani ya Bunge na si kumsusia mbuzi bucha. Tunaenda kukabiliana na CCM mwanzo mwisho kuhakikisha haki inatendeka,” amesema.
Mbali na hilo, Madeleka amesema anaamini uchaguzi huo utafanyika kwa haki na mshindi atatangazwa, huku akitahadharisha wale wanaojiandaa kuiba kura wajipange.
“Ninaamini uchaguzi utakuwa huru. Tangu kuanzishwa kwa mfumo wa vyama vingi 1992, vyama vya upinzani vimekuwa vikishiriki chaguzi na washindi wamekuwa wakitangazwa na tumewahi kufikisha wabunge wengi tu, uchaguzi wa 2025 bado haujafanyika.

“Muda ukifika na uchaguzi ukifanyika, ninaamini mshindi atatangazwa, lakini ni tahadharishe kwa wale wanaohitaji kuiba kura, tutakuwa tumejipanga kulinda kura, tunachohitaji haki itendeke,” amesema.
Sababu ya kuikacha Tabora Mjini
Madeleka amesema awali, kabla ya kuihama Chadema, mipango yake ilikuwa kugombea Tabora Mjini, lakini baada ya kuona Jimbo la Kivule limezawalia na lina changamoto nyingi, amesukumwa kubakia Dar es Salaam.
“Nimepima Tabora Mjini changamoto zao si nyingi kama ilivyo Kivule. Kivule inashida kubwa, wametelekezwa, nataka kugombea hapa kwa sababu hapa ni nyumbani pia,” amesema Madeleka. Ameongeza kuwa Katiba ya Tanzania inaruhusu kila raia kushiriki uchaguzi popote ili mradi awe ndani ya mipaka ya nchi.
“Tabora ni kwetu ila sijawahi kugombea ubunge, lakini nimeipa kipaumbele Kivule kwa sababu ina matatizo mengi, mvua zikianza kunyesha panakuwa kama kisiwa, uongo ukweli?
“Siwezi kuacha kusaidia jimbo lenye matatizo mengi kama Kivule na kukimbilia Tabora na kwa kuwa hakuna sheria inayonizuia, nimekuja rasmi Kivule,” amesema Madeleka.
Mtihani wa Madereka
Madeleka pamoja na kujitosa kuingia kwenye kinyang’anyiro cha kuwania uwakilishi wa wananchi katika eneo hilo, bado anakabiliwa na upinzani kwanza kujua mahitaji ya wananchi na kuwashawishi mbinu gani atatumia kuwasaidia kutatua.

Abdallah Masoud, Mkazi wa Kivule amesema eneo hilo ni miongoni mwa changamoto zinazowasumbua ni usafiri unasababishwa na mtandao wa barabara kuwa mbovu.
“Kivule haifikiki, kuna barabara inatoka Mwanagati, Msongola na Banana hazipitiki hasa mvua zikianza kunyesha, gharama za usafiri zinapaa na kutuongezea ugumu wa maisha,” amesema mwananchi huo.
Hoja inayoungwa mkono na Sarah Neema huku akisema kila wawakilishi wanaowachagua hawaonekani wakati wa shida, ingawa chaguzi zikikaribia wanakuja na maneno mazuri ya kuonyesha wanajua kero zao.
“Safari hii hatutakubali kudanganyika pamoja na kwamba tumepata jimbo jipya lakini tunahitaji kiongozi mwenye dhamira ya kweli katika kutusaidia,” amesema.
Watara anaitaka Kivule
Mbali na mtihani huo, ni upinzani kutoka kwa vyama vya upinzani, mathalani Chama cha Mapinduzi (CCM) na inatajwa Mbunge wa Tarime Vijijini, Mwita Waitara atajitosa katika jimbo hilo ukiwa ni mpango wake wa kuchanga karata kuangalia uwezekano wa kurudi tena mjengoni.
Ingawa Waitara mwenyewe hajaweka wazi nia hiyo, lakini kwa mujibu wa chanzo cha kuaminika kutoka ndani ya CCM, uwezekano wa kurudi Tarime kutetea nafasi ya uwakilishi bungeni ni mdogo kwani anakabiliwa na ushindani mkali na kada mwenzake wa CCM mwenye nguvu na ushawishi.
Si huyo pekee kutoka ndani ya CCM, Naibu Meya wa Jiji la Ilala, Ojambi Masaburi naye anachanga karata zake ili apate fursa kuwawakilisha wananchi hao.

Madereka amesema kutokana na matatizo yaliyopo Kivule, yupo tayari kupambana kutafuta nafasi ya kuwawakilisha kwa kukabiliana na mgombea yeyote kutoka vyama vingine iwapo atapitishwa na chama hicho.