Yanga yamaliza kikao na Bodi ya Ligi, yakomalia ‘hatuchezi’

Muktasari:
- Uongozi wa Bodi ya Ligi Kuu Tanzania (TPLB) na Uongozi wa Yanga wamefanya mkutano leo Jumatatu, Juni 9, 2025 kujadili hatima ya mechi dhidi ya Simba iliyopangwa kuchezwa Juni 15, 2025.
Dar es Salaam. Uongozi wa Yanga umesisitiza kuwa hautocheza mechi dhidi ya Simba, Juni 15, 2025 kama matakwa yake hayatofanyiwa kazi licha ya leo Juni 9, 2025 kufanya kikao na uongozi wa Bodi ya Ligi Kuu Tanzania (TPLB).
Taarifa iliyotolewa na Kamati ya Utendaji ya Yanga leo, imesema kuwa msimamo wao hautobadilika kama wanayoyaomba hayatashughulikiwa.
“Uongozi wa Young Africans Sports Club, unapenda kuutarifu umma kuwa, tarehe 7 Juni, 2025 tulipokea barua kutoka Bodi ya Ligi Kuu Tanzania kwa ajili ya kuhudhuria kikao maalum cha kujadili masuala yahusuyo mchezo namba 184 wa Ligi Kuu ya NBC, YANGA dhidi ya Simba.
“Uongozi wa Klabu yetu ulitii wito huo na kushiriki kwenye kikao kilichofanyika leo, Jumatatu Juni 9, 2025 kwenye ofisi za Bodi ya Ligi Tanzania zilizopo jengo la NSSF Mafao House, Dar Es Salaam, kuanzia saa 4:00 asubuhi.
“Baada ya majadiliano ya saa kadhaa, Viongozi wa Klabu waliwasilisha msimamo wa Klabu yetu kuwa hatutashiriki mchezo namba 184 uliopangwa kufanyika tarehe 15 Juni 2025 mpaka pale matakwa yetu tuliyoyawasilisha kwa maandishi kwao yatakapotimizwa.
“Tunawatakia kila la heri Bodi ya Ligi na Shirikisho la Mpira wa Miguu Nchini katika kushughulikia matakwa yetu yenye mustakabali mkubwa
kwenye maendeleo ya mpira wa miguu Tanzania,” imefafanua taarifa hiyo ya Yanga.
Akizungumza mara baada ya mkutano huo na TPLB uliofanyika katika makao makuu ya Bodi, Ilala, Dar es Salaam, Makamu wa Rais wa Yanga, Arafat Haji amesema klabu yao imeshiriki kikao hicho kuwasilisha msimamo wa wanachama na mashabiki wao.
Akizungumzia juu ya kukubali
kucheza mechi dhidi ya Simba Arafat amesema Yanga haikuwahi kusema kama itacheza mechi hiyo.
"Tumemaliza mkutano na tulichofanya ni kuwasilisha msimamo wa klabu kutoka kwa wanachama na mashabiki wetu hilo ndio kubwa," amesema Arafat Mara baada ya kusema hayo, Arafat aliondoka eneo hilo sambamba na viongozi wenzake.
Ofisa Habari wa Bodi ya Ligi Karim Boimanda amesema taarifa kamili juu ya mkutano huo itatolewa na Afisa Mtendaji Mkuu wa Bodi Almas Kasongo.