Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Mwanaharakati wa Kenya Boniface Mwangi aachiwa huru Tanzania

Muktasari:

  • Akizungumza Mei 19, mwaka huu wakati wa uzinduzi wa Sera mpya ya mambo ya nje (Toleo la mwaka 2024) ukumbi wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNICC), Rais Samia Suluhu Hassan amesema hataruhusu watu kutoka mataifa mengine kuvuruga amani ya nchi.

Nairobi. Mwanaharakati, Boniface Mwangi aliyekuwa anadaiwa kuwekwa kizuizini nchini Tanzania  amepatikana eneo la Ukunda, Kwale nchini Kenya.

Awali, Mwangi na wanaharakati wenzake akiwemo Martha Karua walisafiri kutoka nchini Kenya hadi Tanzania kuhudhuria usikilizwaji wa kesi za Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Tundu Lissu katika mahakama ya Kisutu jijini Dar es Salaam.

Hata hivyo lengo hilo liligonga mwamba baada ya Martha na wenzake kuzuiwa uwanja wa Julius Nyerere (JNIA) huku Mwangi akidaiwa kuchukuliwa na kuwekwa kizuizini.

Hata hivyo, Serikali ya Tanzania haijatoa taarifa yoyote kuhusu madai ya awali ya kumshikilia mwanaharakati huyo hata kuachiwa huru kwake kama inavyodaiwa.

Kwa mujibu wa vyombo vya habari nchini Kenya, Mwangi aliondolewa nchini Tanzania na kusafirishwa kwa barabara hadi nchini Kenya ambako aliachwa eneo la Ukunda nchini humo.

Familia ya mwanaharakati huyo imethibitisha kuachiliwa kwake ikisema kuwa tayari amekimbizwa hospitalini kwa uchunguzi wa kiafya.

Kupatikana kwake kumetokea saa chache baada kuibuka mijadala katika mitandao ya kijamii na taasisi za kiraia na haki za binadamu zikiongeza msukumo wa kuachiliwa kwake.

Awali, akizungumza leo Alhamisi Mei 22, 2025, Katibu wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Kenya, Dk Abraham Korir Sing’Oei amelalamikia kutoweka kwa Mwangi , huku akiiomba Serikali ya Rais Samia Suluhu Hassan, kumwachilia huru.

“Wizara inabaini kuwa licha ya maombi kadhaa, maofisa wa Serikali ya Kenya wamezuiwa kupata taarifa pia kumfikia Mwangi. Wizara pia ina wasiwasi kuhusu hali yake ya afya, ustawi wake kwa ujumla na ukosefu wa taarifa kuhusu kuzuiliwa kwake,” amesema Katibu huyo katika taarifa kwa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki ya Tanzania.

Pia, kupitia taarifa kwa umma iliyochapishwa leo na wizara hiyo imeonyesha wasiwasi kuhusu afya yake na kukosekana kwa taarifa za kuzuiliwa kwake.

Pia jana, mke wa mwanaharakati huyo, Njeri Mwangi, aliaambatana na mtoto wake mkubwa, mama yake na mawakili wake hadi katika ubalozi wa Tanzania nchini Kenya na baadaye kuelekea katika Wizara ya Mambo ya Nje mjini Nairobi, kuelezea hofu kubwa kuhusu hali ya mume wake akitaja kuwa hajazungumza naye tangu Jumatatu alipokamatwa.

"Alikwenda Tanzania kufuatilia kesi ya Lissu (Mwenyekiti wa Chadema) lakini baadaye simu yake ikakatika na nadhani ni hapo ilipochukuliwa. Lakini si kawaida yake, angekuwa amefanya kila awezalo kupata njia ya kuwasiliana na mimi. Ila ni kimya tu. Kwa hivyo nina wasiwasi kwa sababu sijui kama hajiwezi, ameumia au yuko vipi," amesema Njeri.

Njeri aliendelea kusema, "Sio mara ya kwanza Boniface Mwangi kujikuta katika changamoto za kisheria, ila familia yake haijawahi kuwa kama ilivyo sasa anavyozuiliwa nje ya nchi."

"Ningependa kuiomba Serikali ya Tanzania kumrejesha nyumbani na hata kama amekosa, tungependa afunguliwe mashtaka hapa nyumbani, manake nyumbani ni nyumbani. Watoto wana wasiwasi, wananiuliza kila siku alipo baba na sina majibu ya kuwapa. Hata kama atarudi akiwa hali gani, nitakubali, ila tu, namtaka mume wangu arejee nyumbani," Njeri amesema.

Mwanaharakati huyo alikuwa ameripotiwa kwamba ameachiliwa huru na kurejeshwa Kenya siku ya Jumanne, ila Serikali ya Kenya ilithibitisha kwamba alikuwa bado anazuiliwa Tanzania.

Wakati hupo, wanaharakati wa Kenya wameungana na Serikali ya nchi hiyo kulaani hatua ya serikali ya Tanzania kumkamata mwanaharakati huyo.

Akizungumza Mei 19, mwaka huu wakati wa uzinduzi wa Sera mpya ya mambo ya nje (Toleo la mwaka 2024) ukumbi wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNICC), Rais Samia Suluhu Hassan alisema hataruhusu watu kutoka mataifa mengine kuvuruga amani ya nchi.

“Tumeanza kuona mwenendo ambapo baadhi ya wanaharakati kutoka nchi jirani wanajaribu kuingilia mambo yetu. Kama wamekomeshwa kwao, basi wasije kuvuruga amani yetu hapa,” alisema Samia.



OSZAR »