Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Makalla awavaa Chadema Simiyu, adai wanawapotosha wananchi

Muktasari:

  • Kauli hiyo ya CCM imekuja wiki moja baada ya viongozi wakuu wa Chadema wakiongozwa na Makamu Mwenyekiti wa chama hicho, John Heche wakidai Serikali imeshindwa kuwekeza katika kilimo cha umwagiliaji hasa zao la mpunga ndio maana wananchi wanategemea mvua.

Simiyu. Chama cha Mapinduzi (CCM) kimesema Serikali inawathamini wananchi wa Mkoa wa Simiyu, wakiwemo wakulima wa mpunga na pamba, ndio maana imefanya jitihada mbalimbali za kuboresha mazingira ya kilimo cha mazao hayo ili kuyaongezea thamani.

Kutokana na hilo, CCM imewataka wananchi wa Simiyu kupuuza maneno yanayosemwa na baadhi ya viongozi wa upinzani waliodai Serikali haijafanya kitu kwa wakulima wa pamba na mpunga mkoani humo.

Kauli hiyo ya CCM imekuja wiki moja baada ya viongozi wakuu wa Chadema wakiongozwa na Makamu Mwenyekiti wa chama hicho, John Heche wakidai Serikali imeshindwa kuwekeza katika kilimo cha umwagiliaji hasa zao la mpunga ndio maana wananchi wanategemea mvua.

Wakati Heche akieleza hayo, Katibu Mkuu wa Chadema, John Mnyika alidai wakulima wa pamba nchini wanaendelea kudhulumiwa na Bodi ya Pamba Tanzania ambayo badala ya kuwasaidia, imekuwa chanzo cha manyanyaso ya kiuchumi dhidi yao.

Mnyika alidai mbinu wanazozitumia kuwapatia wakulima pembejeo kwa mkopo, kisha kuwalazimisha kuuza mazao yao kupitia Vyama vya Ushirika wa Masoko na Uzalishaji (Amcos), imekuwa ikiwabana.

Akizungumzia madai hayo leo Ijumaa Mei 23, 2024, Katibu wa Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa CCM, Amos Makalla ambaye anaendelea na ziara yake Maswa mkoani Simiyu, amewataka wananchi wa Simiyu kuwapuuza wapinzani kwa sababu CCM inatambua kuwa mkoa huo unapiga hatua kubwa za maendeleo.

Amesema Serikali imetoa fedha za kuboresha bonde la mpunga la Masela ili kuwezesha kilimo cha umwagiliaji cha zao hilo na mpunga kuongeza tija na uzalishaji wa zao hili.

“Wananchi wa Simiyu wanajua zao kubwa la mkoa huu ni pamba, kwa kutambua hilo Serikali imeleta ruzuku kwa wakulima wa zao hili ikiwemo matreka 300 yatumike mkoani humo,” amesema Makalla.

Katika ufafanuzi wake, Makalla amesema matreka hayo bei ya kulima ni Sh70,000 lakini Serikali imetoa ruzuku ambayo itawezesha wakulima kulima kwa Sh35,000.

Mbali na hilo, mwenezi huyo amesema Serikali imeweka ruzuku kwenye pembejeo ili kurahisisha upatikanaji wake kwa wakulima wa mpunga na pamba, huku akiwashangaa wanaosema hakuna lililofanyika katika sekta hiyo.

“Kama hiyo haitoshi wilaya ya Itilima kuna eneo limetengwa kwa ajili ya kiwanda cha kuchakata pamba ili kuliongezea thamani. Hao wanaobeza ni wageni, hawajahi kulima pamba wala mpunga, hawajui chochote bali wanabeza kilichofanyika,” amesema Makalla.

Mbali na hilo, Makalla alimpongeza mbunge wa Maswa Magharibi, Mashimba Ndaki kwa namna anavyotekeleza majukumu yake ya kuwahudumia wananchi wa jimbo hilo, akisema ana upiga mwingi na kumtakia kila heri katika safari yake.

Tunzeni kitambulisho cha mpigakura

Tangu kuanza ziara yake mkoa wa Simiyu jana Alhamisi Mei 22, 2025, Makalla amewataka wananchi kutunza kitambulisho cha mpigakura ili kukitumia katika uchaguzi mkuu utakaofanyika Oktoba 2025.

“Uchaguzi upo kama kawaida na utasimamiwa na Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC), naomba mpuuzee maneno yanayosemwa eti uchaguzi utazuiwa, msiwasikilize hawana hoja hao,” amesema Makalla.

Mbunge wa Jimbo la Maswa Magharibi, Ndaki, amesema uboreshaji wa skimu ya bonde la mpunga la Masela ni hatua muhimu na jitihada za Serikali kuboresha sekta ya kilimo na kuongeza usalama wa chakula nchini.

Ndaki amesema hivi karibuni Serikali iliridhia kutolewa kwa Sh4 bilioni ili mchakato wa ujenzi wa bonde hilo uanze na tayari mkandarasi atakayeteleza jukumu hilo ameshapatikana, sio muda mrefu atakwenda kuripoti wilayani Maswa.

Ndaki, aliyewahi kuwa Waziri wa Mifugo na Uvuvi, amewataka wananchi wa Maswa na Simiyu kumpa kumuunga mkono mgombea wa urais wa CCM, Samia Suluhu Hassan ambaye Serikali anayoingoza imepeleka miradi mbalimbali ya maendeleo mkoani humo.


OSZAR »